BBC Swahili Narcolepsy Feature

Narcolepsy: Hali inayokufanya ulale kila wakati

Kulala ni jambo la kawaida, lakini utamchukulia vipi mtu anapopatwa na usingizi wa ghafla.

Hili ni tatizo la kiafya linalojulikana kama Narcolepsy.

Kwa kawaida binadamu hulala kuanzia masaa ya usiku , japo kuna wengine ambao kutokana na kazi hulala mchana.

Watch Video: BBC Swahili Narcolepsy Feature

Lakini hebu tafakari kuwa na ugonjwa wa kila mara wa kupata usingizi kwa ghafla ukiwa katika shughuli zako za kila siku ? ndio hali anayoishi nayo Mwalimu Simon Njenga Gakuna.

Ana Miaka 47 na tangu kuzaliwa kwake anakumbuka akijipata kichakani akiwa amelala.

Hii ni hali ambayo mkewe Simon, Bi Caroline Njenga amekuwa akiishuhudia kwa mumewe.

Ugonjwa wa kulala?

Lakini je ugonjwa ama hali anayoipitia Simon ni kitu gani haswa?

Matibibu wanaiita hali hii Narcolepsy. Ni hali ambayo inamkumba mtu na kushindwa kujizuia kulala kila wakati .

Hali hii kulingana na Daktari William Kiuna kutoka Kaunti ya Nakuru Kaskazini Magharibi mwa Kenya inawaathiri wanaume wengi kuliko wanawake.

Hali hii ya kulala mtu huzaliwa nayo.

Kwake Simon anasema kuwa imebidi aizungumzie hali yake kimasomaso ili jamii iweze kuelewa kuwa wakati mwengine unapokutana na mtu anayelala kila wakati inaweza kuwa anaugua hali ya Narcolepsy

Changamoto za hali hii ya kulala ni zipi ?

Mara kwa mara Bwana Simon amejipata katika hatari hususan kwa kuwa yeye anamiliki gari na huliendesha kila wakati.

Katika kisa kimoja alielezea kuwa alijipata amesimamisha gari katikati ya barabara na kupitwa na usingizi hadi usiku wa manane , vile vile akiwa kwenye darasa kwa kuwa yeye ni mwalimu wa sayansi na hesabati amejipata akiwa amelala huku wanafunzi wakiwa wanasubiri awafunze.

Simon anasema, ‘mara kwa mara watu hudhani mimi ni mraibu wa kulewa kwa kuwa hata katika mkutano mashuhuri hali ya kulala ikija huwa sina cha kufanya ila kusalimu amri’.

Anasema kuwa kabla ya kushikwa na usingizi huu wa ghafla huanza kuhisi hali ya joto kisha mishipa yake huanza kuwa moto kabla ya usingizi kumpata.

Ugonjwa huu wa narcolepsy hauna tiba, na madaktari wanasema kuwa ni dawa tu ambazo mtu hupewa ilikuihimili hali hii.

Wanawe Simon, Antony Gakuna na Mitchel Wambui wanasema kuwa wameielewa hali ya baba yao, na licha ya kukabiliwa na unyanyapaa kutoka kwa jamii wao wanajivunia baba yao mzazi.